Saturday, August 12, 2017

MANYWANYWA – MAJANI CHAKULA CHA KUKU

Manywanywa ni jina la majani maarufu sana hapa kwetu lushoto. Pengine ni aina ya mmea ama majani ambayo hujulikana kwa majina mbalimbali kutokana na aina na jamii ya mimia hiyo. Kuna uwezekano mkubwa majani haya kutambulika kwa majina ama jina tofauti na ''Manywanywa''. Uwezekano huo ni kutokana na mahali, tamaduni, sayansi ya utambuzi wa mimea au matumizi ya majani haya katika jamii fulani.

Majani yanayotambulika kama Manywanywa, ni majani pori yanayoota aghalabu maeneo ya porini yenye baridi na mwinuko mfano katika milima na miinuko. Hapa lushoto, hujiotea katika maeneo mengi na si majani ya kupanda. Wenyeji na wakazi wa lushoto, huyatumia majani haya kwa matumizi mbalimbali nyumbani.




Kwanza manywanywa hutumika kuondoa utomvu (waweza kuwa ni utomvu wa matunda, mboga au miti). Mfano mtu aliyekula tunda la fenesi au kumenya ndizi mbichi, mikono yake ipatapo utomvu; anaweza kuchuma manywanywa na kufikicha katika mikono yake yenye utomu. Kutokana na majani haya kutoa aina fulani ya majimaji, basi utomvu huo unaanza kuondoka taratibu mithili ya mtu anayejisafisha kwa sabuni. 


Pili manywanywa hutumika kuondoa ukakasi katika na hali ya kufa ganzi katika meno. Endapo mtu atakula kitu,chakula ama matunda mfano embe mbichi; na kupata ukakasi katika meno yake, anaweza kutafuna sehemu ya majani haya na kuondokana na hali ya ukakasi na kufa ganzi kwa meno yake. 

Tatu manywanywa hutumika kama chakula cha kuku. Ndio hapa lushoto, maeneo mengi wafugaji wa kuku wamekuwa wakiyatumia manywanywa kama chakula mwambata cha kuku. Mbali na pumba za nafaka, mashudu na vyakula maalumu vilivyoandaliwa kwa kulishia kuku, pia manywanywa hutumika kulisha kuku. 

Kama chakula cha kuku, manywanywa husemekana kuwa na kiwango kikubwa cha madini, vitamini na virutubisho muhimu kwa ukuzaji wa kuku. Majani haya hutumika kulisha kuku wa aina zote ( wa kisasa na wa kienyeji). Manywanywa yana vitamini ya kutosha na muhimu kwa ukuzaji wa kuku kama majani mabichi mengine (Lusina, Majani ya mpapai na Mchicha). 

Katika ukuaji, kuku huhitaji kiwango kikubwa cha madini ya fosforasi na calcium (metali laini nyeupe ambayo hupatikana katika unga wa dagaa na mifupa ya wanyama iliyochomwa na chokaa maalum ya kuku – madini haya hupatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo), ambayo ina kazi ya kurutubisha mifupa nakusaidia uzalishaji wa mayai kwa kuku wanaotaga kuwa na mayai yenye ganda (kaka) gumu na kiini chenye unjano mwingi. 

Hutokea katika mayai ya kuku wa kisasa kuwa na hafifu ya unjano kaika mayai, lakini endapo kuku hao wa kisasa wakalishwa manywanywa, mabadiliko ya unjano katika mayai yao huongezeka na kuwa mithili ya mayai ya kuku wa kienyeji. 

Katika ufugaji wa kuku, mfugaji anashauriwa kuwa mbunifu, kuzingatia kanuni za ufugaji bora pamoja na kutumia gharama ndogo (matumizi yasizi mapato) ili kukuza kipato chake kwa kufuga kwa tija. Hivyo ni muhimu mfugaji akatumia mazingira yake yanayomzunguka na kutumia vitu asili katika shughuli zake za ufugaji wake. 

Keibuni lushoto 


Lushoto Rise-Up 
Gunda W. C. 
August, 2017.

0 comments:

Post a Comment